Kutana na Mama N

IMG-20170312-WA0011Katika harakati za kuwatembelea wahitaji katika Jiji la Dar-es-salaam hivi majuzi mimi na mke wangu tulikutana na ombaomba kadhaa, wengi wao wakiwa hawana chakula wala makazi.

Najua kila mmoja wetu ana maoni yake kuhusu ombaomba hawa waliotapakaa  kila kona ya Jiji letu. Wako wanaofikiri kwamba ndugu hao wako mtaani kwa kuwa wanapenda – yaani ni fani yao. Wapo pia wanaoamini kwamba watu hao hawastahili kusaidiwa kwa kuwa wana utamaduni ama tabia ya uvivu kwani kuna watu wengine wenye hali kama zao (ama mbaya zaidi) lakini wanajishughulisha na kujipatia kipato chao wenyewe.

Kwa kweli mimi sipingani na sababu hizo kwani zina ukweli kiasi fulani. Lakini kikubwa ni kwamba sio kila mtu anayejitosa mtaani anapenda kufanya hivyo. Naamini kuna wengine wanalazimika kumeza kiburi, aibu na changamoto zinginezo ili kukaa mtaani kuomba kwa kuwa hawana jinsi kabisa. Mfano mzuri ni  Mama N (sio jina lake kamili) tuliyekutana naye mtaani hivi majuzi.

Mama N alitelekezwa na mume wake akiwa mjamzito huku tayari akiwa na mzigo  wa kumlea mtoto mwingine mdogo. Baada ya mume wake kughiribiwa na mwanamke mwingine Mama N alilazimika kulea mimba yake  mpaka alipojifungua bila msaada wowote wa kimatunzo kwani hakuwa na chanzo kingine cha mapato. Hali hii ilimfanya Mama N (pichani juu) kujitosa mtaani kuomba pesa za kutunza watoto wake wawili – wa mwisho akiwa na umri wa mwezi mmoja na nusu tu. Pamoja na kwamba watu kadhaa wamejitokeza kumsaidia bado misaada hiyo haitoshi na siyo ya uhakika.

Ni vizuri nidokeze kuwa Mama N ni Mkristo mwaminifu. Pamoja na hali aliyonayo bado anakwenda kanisani na tulipokutana naye ndio alikuwa ametoka ibadani na biblia yake iliyokuwa imefunguliwa ilikuwa pembeni yake.

Watu kama Mama N ni watu wa kawaida wenye hisia, aibu na matamanio ya maisha kama sisi sote. Tunapishana nao mitaani na wengine tunakaa na kuabudu pamoja no makanisani. Lakini ni wahitaji na ni wajibu wetu kuwasaidia.

Kristo alisema, “Kisha Mfalme atawaambia wale walioko mkono wake wa kuume, Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu; kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha; nalikuwa uchi, mkanivika nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nalikuwa kifungoni, mkanijia. Ndipo wenye haki watakapomjibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona una njaa, tukakulisha, au una kiu tukakunywesha? Tena ni lini tulipokuona u mgeni, tukakukaribisha, au u uchi, tukakuvika? Ni lini tena tulipokuona u mgonjwa, au kifungoni, tukakujia? Na Mfalme atajibu, akiwaambia, Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.” – Matayo 25:34-40

Maandiko hayatutaki kujua sababu za uhitaji (kwamba ni uvivu au vinginevyo) kabla ya kukidhi uhitaji tunaouona. Anachoangalia Kristo ni kwamba umekidhi uhitaji na atakubariki vilivyo.

Najua sio kila mtu anaweza kuwa na muda wa kuwatembelea wahitaji hawa lakini kila mmoja wetu anaweza kufanya kitu. Ndiyo maana Dream Life Mission imeanzisha huduma ya Kimbilio.

Unaweza kukidhi mahitaji ya wapendwa wetu hawa na ukajizolea baraka kwa kutoa chochote ulichonacho na sisi tutauwasilisha unapohusika. Tafadhali wasiliana nasi ili kupata habari zaidi juu ya huduma hii kwa kubofya hapa.

Mungu akubariki sana.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: