SIMONI MKIRENE

 simon-of-cyreneNi jambo la kusikitisha kuona kwamba Watumishi wa Mungu (namaanisha watumishi wa kweli na sio wasanii) wanapitia kipindi kigumu sana. Wengi wana changamoto za kifedha, kiafya na kihuduma. Changamoto hizi zote zinapelekea kuyumba kwa familia na mpasuko wa ndoa zao. Wengi wanatumika huku mioyo yao ikiwa majeruhi. Majeraha hayo yamewafanya wengine wakimbie huduma ama kurudi nyuma kabisa.

Tatizo hili liko duniani kote sio Tanzania tu. Utafiti unaonyesha kwamba nchini Marekani asilimia 80 ya Watumishi na asilimia 84 ya wenzi wao wana matatizo ya msongo wa mawazo (depression). Kila mwezi zaidi ya Wachungaji 1,500 wanakimbia huduma kwa sababu hizo hizo.

Kinachosikitisha zaidi ni kwamba watumishi wanapitia changamoto za kimaisha na za kiutumishi kwa siri tena peke yao. Inasemekana kwamba asilimia sabini ya watumishi hawana rafiki wa karibu. Wengi wana watu wanaoshirikiana nao kihuduma lakini ni wachache wenye marafiki wa kusaidiana mapito ya kibinafsi.

Watumishi wanapitia changamoto hizi kwa siri kwa sababu wamejiaminisha kwamba Mtumishi wa kweli hapashwi kupitia changamoto fulani fulani. Wengi tunaamini kwamba changamoto ni matokeo ya dhambi au mtindio wa Imani. Sasa changamoto hizohizo zinapotukumba hata sisi watumishi tunaghafilika. Kinachofuata ni kuficha ili tusionekane kuwa sisi nasi “tumetenda dhambi” au “tumepungukiwa Imani.” Tunajificha kwa kuamini kwamba udhaifu wetu ukijulikana tutadharauliwa, tutatengwa au tutapoteza kabisa huduma.

Ukweli ni kwamba hakuna aliye na leseni ya kukwepa changamoto. Utumishi, utakatifu au imani thabiti sio kinga ya kila changamoto. Nachelea kusema kuwa mara nyingi utumishi, utakatifu na imani thabiti ni vyanzo vya changamoto. Ni kweli kwamba changamoto zingine ni matokeo ya dhambi ama ukosefu wa imani. Lakini ni kweli pia kwamba changamoto zingine tunazipitia kwa sababu tu watumishi , tu wenye haki au kwa sababu ya imani yetu. Maandiko yanasema kwamba mateso ya mwenye haki (hususan watumishi) ni mengi lakini Bwana ameahidi kutusaidia kuyashinda yote ( Zab. 34:19; Yoh 16:33).

Washirika wanapokumbwa na matatizo wanamkimbilia Mchungungaji. Licha ya majukumu mengine ya kibinafsi, ya kifamilia na ya kihuduma wachungaji wanategemewa kubeba mizigo ya matatizo ya watu. Mara nyingi watumishi hawa hawana muda maalum wa kutimiza majukumu haya, wako kazini masaa 24 siku saba kwa wiki. Lakini Watumishi wenyewe wanapopata matatizo hawana pa kukimbilia.

Baadhi ya watumishi wanapitia matatizo peke yao kwa kufikiri kwamba hawahitaji msaada kutoka kwa mtu yeyote. Lakini kuna Watumishi wengine wanaotamani kuwa na mtu wa kuwaelewa, kuwafariji na kuwasaidia lakini wanakosa msaada.

Wote tunahitaji rafiki. Hata Kristo alikuwa na marafiki [Yoh. 15:15]. Hakuna mtu anayeweza kushinda mapito peke yake. Kila binadamu – bila kujali kwamba ni Musa, Elia, Paulo au Petro – anahitaji msaada wa wengine ili avuke mapito kwa ushindi.

Nasema hata Bwana wetu Yesu alipokuwa Getsemane alihitaji ushirika na maombi ya wanafunzi wake – Petro, Yohana na Yakobo ( Marko 14:32-42). Kristo hakubeba msalaba peke yake, alisaidiwa na Simon Mkirene kutoka Afrika (Libya) kubeba msalaba. Kama Kristo Yesu mwenyewe alihitaji msaada wa Simoni Mkirene kila mtu anamhitaji Simoni Mkirene.

Maombi yangu ni kuwa wale wote wanaopitia kipindi kigumu Bwana awapelekee Simon Mkirene. Na kwa sisi wengine Bwana atupe utayari na wepesi wa Simoni Mkirene. Kila mmoja wetu awe radhi kuwabebea wengine mizigo na kulia na wale waliao. Hii ni pamoja na kuwaombea wanaopitia changamoto na kwa kukidhi uhitaji wao.

Huduma mojawapo ya Simon Mkirene ni kusambaza ujumbe huu kwa watu wengi kwa kadri inavyowezekana. Tafadhali fanya hivyo sasa kwani kunamtumishi amekata tamaa na anahitaji ujumbe huu ili atiwe moyo kuendelea na safari ya utumishi. Kwa kufanya hivyo utapokea sehemu ya nyara za ushindi wa msalaba. Amen

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: