SIRI YA USHINDI

battlestamfordbridgeMfalme Daudi anashikilia rekodi ya kupigana vita zaidi ya 66 bila kushindwa hata mara moja. Moja ya siri kubwa za ushindi wake ni kuchagua vita vya kupigana.

Ni dhahiri kwamba Mfalme Daudi alikuwa jasiri na hodari wa vita, lakini hakupigana na kila adui. Kuna alioamua kuwapuuza na kuna aliowakimbia. Mifano mizuri ni ya Eliab, Sauli, Ishbosheth, na Absalom.

Eliab na wadogo zake walimchukia sana Daudi, mdogo wao wa mwisho, lakini Daudi hakuwahi kugombana nao hata pale alipochokozwa.

Mfalme Sauli na ukoo wake wote (isipokuwa Jonathan) walipenda Daudi afe ili kukilinda kiti chao cha Ufalme wa Israel. Lakini pamoja na kujua kwamba Mfalme Sauli alishatenda dhambi; Mfalme Daudi alijua kwamba Mungu alishamuacha Mfalme Sauli na kumteua yeye Daudi kuchukua nafasi yake; pamoja na kuwa na uwezo na fursa nyingi za kummaliza Mfalme Sauli  Mfalme Daudi hakudiriki kunyoosha mkono wake dhidi ya mtu aliyemuita “mpakwa mafuta wa Bwana”. Hata baada ya kusikia kwamba Mfalme Sauli amekufa Daudi aliomboleza na kumtungia shairi la majonzi. Si hivyo tu Daudi alidiriki hata kumuua mjumbe wa habari  “mbaya” za kifo cha Mfalme Sauli. Mfalme Daudi pia aliwaua akina Baanah and Recab waliomuua Ishbosheth mtoto wa Mfalme Sauli kwa kufikiri kwamba kwa kufanya hivyo wangemfurahisha yeye Mfalme Daudi.

Absalom aliasi na kujitangazia ufalme dhidi ya Daudi baba yake. Hii ilikuwa baada ya kulala na wake za Daudi Mfalme mchana, ghorofani, mbele ya kadamnasi. Lakini aliposikia juu ya uasi wa Absalom na kwamba alikuwa na njama za kuvamia ikulu na kumuua Daudi alitimua mbio. Hata baadae alipoidhinisha jitihada za kumzuia Absalom asiendeleze uasi dhidi ya Mungu na kuleta madhara makubwa zaidi kwa taifa Daudi alitoa amri kali kwa makamanda wake ya kuhakikisha Absalom anaachwa hai na salama.

Ukiangalia kwa makini utagundua kwamba Mfalme Daudi alikwepa kupigana na ndugu zake. Kila vita aliyochagua kupigana ilikuwa dhidi ya maadui wa Mungu wake au watu wake. Mfalme Daudi hakupigana vita kulinda maslahi yake binafsi, alipigana na wenye nguvu ili kutetea maslahi ya wengine, hususan wanyonge, kwa utukufu wa Bwana. Mfalme hakujipigania, alimuachia Mungu apigane na maadui zake binafsi.

Umahiri wa kivita hauko kwenye ushindi peke yake. Umahiri wa kivita unategemea unapigana na nani na kwanini. Umahiri wa kivita hauko kwenye kupambana dhidi ya ndugu zako waliowanyonge. Umahiri wa kivita uko kwenye kupigana “kiume” dhidi ya wenye nguvu ili kutetea maslahi ya wanyonge.

Umahiri wa mfungaji bora hauko kwenye kufunga magoli dhidi ya timu yako; mfungaji mahiri ni yule anayefunga magoli mengi dhidi ya timu pinzani yenye ulinzi dhabiti.

Sifa kuu ya kiongozi mahiri, ni kutetea maslahi ya watu waliochini ya dhamana yake. Jukumu kuu la kiongozi ni kuhakikisha maisha ya wale aliopewa dhamana ya kuwaongoza yanakuwa bora na salama.

Bila kujali alikuwa na dhamana ya kuchunga kondoo au binadamu Mfalme Daudi alitoa uhai wake kupambana na chochote kilicho hatarisha usalama wao.

Bwana Yesu alisema, “Adui huja ili aibe, aue na kuteketeza. Lakini mimi nimekuja ili wapate uzima tele. Mimi ni mchungaji mwema. Tofauti na mchungaji wa ujira, Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wake. Mchungaji wa ujira sio mmiliki wa kondoo. Ndio maana akimuona mbwa mwitu anakuja hukimbia na kuwaacha kondoo. Kisha mbwa mwitu huwashambulia kondoo na kuwatawanya. Mchungaji wa ajira hukimbia kwa sababu anajali maslahi yake zaidi kuliko maslahi yakondoo. (Yohana 10:10-13)

 

protectyouridea1-2
jukumu kuu la kiongozi ni kulisha na kulinda walio chini yake, hususan wanyonge

Kwa bahati mbaya viongozi wengi katika jamii yetu (hii ni pamoja na makanisani) hatujali maslahi ya watu wetu. Tunatumia raslimali za watu tuliopewa dhamana ya kuwaongoza kujipatia maslahi yetu badala ya kutumia raslimali zetu kwa maslahi ya watu wetu. Ni mara ngapi tumeshuhudia viongozi wetu wakitumia silaha kali dhidi ya watu wao – wengi wao wakiwa wanyonge – ili kutetea maslahi yao. Badala ya kuwatetea wasiojiweza tumejigamba kujitajirisha kwa kutumia mali za masikini.

Moja ya uhaini wa kivita ni kuwashambulia watu wasiokuwa na uwezo wa kujitetea. Ndio maana Kristo alisema, yeye hajali mtu akisema neno baya dhidi yake, lakini akasema atakayemkufuru Roho Mtakatifu (sehemu ndogo na laini zaidi ya UTATU Mtakarifu) hatasamehewa. Kwa hiyo dhambi kuu kuliko zote (isiyokuwa na msamaha?) ni kupigana na watu wako na kuwanyanyasa waliodhaifu zaidi kuliko wewe. (Matayo 12:32;Mark 3:23-30).

Wenye busara wanalinda wanyonge kwa sababu wanajua hao ndio wa muhimu zaidi. Biblia inasema kwamba vitu vinavyoonekana kama vinyonge ndio vitu vyene umaana zaidi. Mtume Paulo anasema sehemu za mwili zilizo dhaifu zaidi ndizo zilizo muhimu zaidi. Tena, viungo vile tunavyovifikiria kuwa havistahili heshima kubwa, ndivyo tunavyovitunza kwa uangalifu zaidi; viungo vya mwili ambavyo ni vya muhimu zaidi havionekani kwani hufichwa kwa makini zaidi. Mungu huvipa heshima na umuhimu mkubwa zaidi vitu ambavyo wengi wanavidharau. (1Kor 12:22-24)

Ukifungua minyororo ya  waliofungwa kwa ukatili na kuwaweka huru walioonewa; ukila chakula chako na wenye njaa na kuwapatia hifadhi maskini wasiokuwa na makao , ukimvika nguo aliye uchi, na usipo wakimbia ndugu zako…nuru yako itachomoza kama mapambazuko na uponyaji wako utatokea haraka; haki yako itakutangulia mbele yako, na utukufu wa Bwana utakufuata nyuma yako ukulinde…. (Isaya 58:6-8)

Ukitaka kuheshimiwa na Mungu waheshimu wanaodharauliwa na watu. Ukitaka nguvu za kimungu wapiganie wasio na nguvu. Ukitaka Mungu akutetee dhidi ya maadui zako watetee wanyonge.

Ukitaka kushinda kila vita, usipigane na kila mtu; usipigane kutetea maslahi yako na kamwe usipigane dhidi ya ulioitwa kuwatumikia au walio damu moja nawe!

Amina.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: