Moja ya matokeo ya kupooza (paralysis) ni kushindwa kuhisi maumivu. Kwamba mwili unashindwa kuhisi maumivu haimaanishi kwamba mwili hauumii. Uharibifu unaweza kuwepo lakini mfumo wa fahamu unaohusika na utambuzi wa uharibifu huo unakuwa na hitilafu. Maumivu sio uharibifu bali ni ishara ya uharibifu. Kuhisi maumivu katika sehemu yoyote ya mwili kunaashiria uharibifu katika sehemu hiyo unaohitaji kurekebishwa. Kwa hiyo maumivu ni sehemu ya mfumo wa asili wa ulinzi unaousaidia mwili kuhisi, kuepuka au kurekebisha matatizo.
Ubinafsi ni dalili ya kupooza kiroho na kimaadili (spiritual – moral paralysis). Kupooza huku kunapelekea watu kutojali mateso ya wengine kunakotokana na kupoteza hisia za maumivu ya wengine. Mateso na vilio vya watoto, yatima, wajane, wazee, walemavu ,masikini na wasiojiweza miongoni mwetu ni makali, yamekuwepo kwa muda mrefu na yanazidi kuongezeka. Cha kushangaza ni jinsi gani Kanisa na jamii kwa ujumla tusivyoguswa na mateso haya.
Jamii ni mwili na kila mwana jamii ni kiungo cha muhimu katika jamii hiyo. Kiungo kimoja , hata kama kina afya kiasi gani, kinategemea viungo vingine ili kuendelea kuwepo. In fact, kiungo kimoja kikiumwa mwili wote unaumwa.
Upendo ni kuumizwa na mateso ya wengine kunakokusukuma kufanya kitu kukomesha mateso hayo.
Biblia inasema sisi (Kanisa) ni Mwili wa Kristo na upendo unapaswa kuwa DNA ya kanisa [Yohan 13:34-35; 1Wakor. 12 -13]. Maumivu ya mmoja wetu ni maumivu yetu sote. Mafanikio ya pamoja ni muhimu kuliko mafanikio yetu binafsi. Kitendo cha kuhujumu mafanikio ya wengine kwa manufaa yako ni sawa na kuwa juu ya mti na kuanza kukata tawi ulilolikalia, likikatika ujue kwa hakika utadondoka nalo.
Maandiko yanatuonya kwamba wasiojiweza na wanaoteseka miongoni mwetu ni viungo muhimu zaidi vinavyohitaji matunzo makini zaidi. Ndio maana kwenye mwili uliotimamu kiungo kimoja kinapougua – bila kujali ni kidogo kiasi gani – mwili wote unaugua na kusimamisha shuguli zingine zote mpaka kiungo kigonjwa kimepona.
Wanaofikiri kwamba mateso ya wengine hayawahusu ni ushahidi wa kutosha kwamba wanaumwa, mioyo yao imekufa ganzi. Nao pia wanahitaji uponyaji.
Yesu Kristo anaumia pamoja na waumiao na wote tuliowazima kiroho hapa duniani tunajisikia kuumia sana. Bibilia inasema hakuna kitakachotutenga na mapenzi ya Mungu, hii ikiwa ni pamoja na mateso. Kristo anajali kwa sababu naye pia anaumia; anaumia kwani yeye ni mwenzetu.
Mateso ya wasiojiweza ni mateso yetu, maumivu ya wagonjwa ni maumivu yetu, vilio vya wajane ni vilio vyetu.
Dream Life Mission kwa upande wetu tumeanzisha huduma ya Kimbilio la wasiojiweza hususan watoto, vijana na akina mama. Kwa kushirikiana na makanisa, mashirika yasiyo ya kiserikali, taasisi za umma, Serikali na watu binafsi Kimbilio linatoa huduma zifuatazo:-
Mahitaji ya dharura ya kujikimu kama vile chakula, mavazi, na makazi; mafunzo, ushauri na uwezeshwaji ili kuwaongezea walengwa uwezo wa kufanya kazi au biashara ili kujiletea maendeleo yao na ya jamii kwa ujumla; Mafunzo ya uongozi kuwawezesha vijana na akina mama kushiriki katika majukwaa ya utoaji wa maamuzi yanayoathiri maendeleo ya jamii. Mafunzo, ushauri, maombi na maombezi ili kuwawezesha kujitambua, kujithamini, kujiamini na kufanya maamuzi sahihi kielimu,kiroho, kisaikolojia, kiafya, kijinsia, na kimahusiano.
Kama kweli nawe unaumia Kristo hebu tuungane na Kristo kuponya maumivu ya wenzetu.