Tanzania ni moja kati ya nchi zenye idadi kubwa zaidi ya watoto na vijana duniani. Cha kusikitisha ni kwamba vijana na watoto hawa ndio wanaokabiliwa na umasikini uliokithiri kutokana na ukosefu wa kazi na malezi mabaya.
Takwimu zinaonyesha kwamba idadi ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi imeongezeka mara mbili kutoka watu milioni 12 mwaka 1990 hadi kufikia watu milioni 25.8 .Kati ya nguvu kazi hiyo asilimia zaidi ya 65 ni vijana wenye umri kati ya miaka 15-34.[1]
Kila mwaka, vijana wapatao 800,000 huingia kwenye soko la ajira linalozalisha si zaidi ya ajira mpya 40,000[2]. Hii ina maana kwamba vijana wengi wanakosa ajira kitendo kinachowafanya vijana wengi kukimbilia mijini ili kujitafutia riziki. Kutokana na maisha ya mijini kuwa magumu vijana wengi hujikuta wakiishi katika mazingira hatarishi na ya kimasikini.
Jitihada za kutosha za kupunguza umasikini zimefanywa na Serikali ya Tanzania chini ya Mkakati wa Taifa wa Ukuaji na Kupunguza Umaskini yaani MKUKUTA . Kutokana na utekelezaji wa Malengo ya Taifa ya Maendeleo ifikapo mwaka 2025 Pato la Taifa limeongezeka mara mbili katika kipindi cha miaka kumi kutoka $ 21.5 bilioni mwaka 2007 hadi $ 47.4 bilioni mwaka 2017.[3]
Aidha jidihada zaidi zinaendlea kuchukuliwa kuifanya nchi yetu iwe ya viwanda ili kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Serikali ya sasa, chini ya Mh. Rais, Dr. John Pombe Magufuli, imepitisha sera inazozitaka Halmashauri kutenga angalau asilimia 10 ya mapato kwa ajili ya uwezeshaji wa vijana, akina mama na watu wenye ulemavu kujipatia ajira. Ni dhahiri kwamba sera hizi zikitekelezwa ipasavyo tatizo la ajira na umasikini nchini Tanzania litapungua.
Pamoja na jitihada hizi za dhati Tanzania bado ni moja ya nchi maskini zaidi duniani. Watoto, vijana, na akina mama wanaendelea kuathiriwa zaidi na umasikinu huu. Utafiti uliofanywa na Tanzania Integrated Labor Force Survey (ILFS) kwa kushirikiana na Shirika la Kazi Duniani (ILO) umedhihirisha kwamba vijana na akina mama hawana ujuzi , elimu na uzoefu unahitajika kuwawezesha kujiletea maendeleo yao na ya Taifa .
Ukosefu wa ajira, umasikini na unyanyaswaji tayari ni matatizo makubwa kwa watoto, vijana na akina mama. Ukijumlisha matatizo mengine kama madawa ya kulevya, mimba za utotoni, na magonjwa hatari kama UKIMWI idadi ya watoto yatima na wajane wasiojiweza itaendelea kuwa kubwa.
Ukubwa wa matatizo yanayowakabili watoto, vijana na akina mama, uwezo mdogo wa serikali kiuchumi na miundo mbinu dhaifu ya ustawi wa jamii ni wazi kwamba nguvu zaidi inahitajika ili kutatua matatizo haya.
Hii ni ni moja tu ya sababu zinazotusukuma kuanzisha KIMBILIO.
Kimbilio, ni kituo maalum cha Kristo kinacholenga kutoa huduma za bure, za kitaalum, na kwa wakati wote ili kutokomeza umaskini na unyanyasaji kwa watoto na vijana bila kujali tofauti za dini au itikadi za kisiasa.
Kama kituo cha aina yake hapa nchini Tanzania, Kimbilio kitawahusisha wana jamii, Serikali za mitaa, taasisi za umma, mashirika yasiyo ya kiserikali, sekta binafsi, Serikali ya Tanzania, na Taasisi zinginezo ili kufikia matokeo yafuatayo:
Mahitaji ya Dharura: Kukidhi mahitaji ya dharura ya kujikimu kama vile chakula, mavazi, na makazi kwa vijana wanaoishi katika mazingira hatarishi au ufukara. Huduma hii itakayotolewa muda wote kwa wahanga kufika kituoni, kwa njia ya simu au kupitia kwenye mtandao unalenga katika kuokoa maisha ya watoto na vijana, kuwafanya vijana wajisikie wako salama, na kwamba wao pia ni watu wa maana.
Kituo cha Kazi. Kutoa mafunzo, ushauri na uwezeshaji kwa vijana ili kuwaongezea uwezo wa kufanya kazi na kujiletea maendeleo yao na ya jamii kwa ujumla.
Biashara Hub. Kutoa mafunzo, ushauri na uwezeshaji kwa vijana ili waweze kuanzisha au kupanua biashara zitakazoboresha jamii.
Kituo cha Uongozi: Kutoa mafunzo, ushauri na uwezeshaji kwa vijana ili waweze kushika hatamu za uongozi kwa kushiriki katika majukwaa ya utoaji wa maamuzi yanayoathiri maendeleo ya jamii.
Stadi za Maisha: Kutoa mafunzo, ushauri, maombi , maombezi na uwezeshaji kwa vijana ili waweze kujitambua, kujithamini, kujiamini na kufanya maamuzi sahihi kiuchumi, kiroho, kisaikolojia, kiafya, kijinsia, na kimahusiano katika nyanja za kibinafsi, kifamilia na kijamii.
Ili lushiriki katika huduma na baraka ya Kimbilio utoaji wako katika moja ya maeneo haya ni muhimu.
VYAKULA NA VINYWAJI
Vinywaji na vyakula visivyo haribika haraka (mfano vyakula vya makopo, nafaka, unga, maji, mafuta, sukari, chumvi nk)
MAVAZI
Tunakusanya nguo, viatu, mitandio n.k
MALAZI
Tunahitaji magodoro, mashuka, vitanda nk
MAKAZI
Tunahitaji nyumba, vyumba au mahali salama pa kulala / kukaa
GROCERIES
Tunapokea vitu kama Sabuni, miswaki, dawa za miswaki, mafuta ya kujipaka nk
PESA
Weka NBC Akaunti Na 033103010960 (Hundi ziandikwe kwa jina la DREAM LIFE MISSION)
TIGO-PESA: 0717179883 (Jina: DREAM MISSION)
M-PESA: 0763320505
WATENDA KAZI : Tunahitaji Waalimu, Washauri, Wataalam mbalimbali kama wanasheria, wahasibu, madaktari, wauguzi, wanamaombi, wasambazaji n.k. Kama unataka kufanya kazi pamoja nasi tafadhali jiandikishe hapa
KAMA UKO TAYAFI KUTOA CHOCHOTE TAFADHALI JAZA FOMU HAPA
_____________________________
[1] National Bureau of Statistics, “Integrated Labor Force Survey: Analytical Report” (Tanzania: National Bureau of Statistics, 2015)
[2] Ibid
[3] World Bank. Databank. https://data.worldbank.org/country/tanzania