BACK TO PENTECOST

Copy of BACK TO PENTECOST copyApril 11 2017

Watumishi na Wakristo wenzangu, shalom.

Kristo Yesu analiasa Kanisa lake kurejea katika msingi wa upendo, kushika hatamu za kiuchumi na kuwajali masikini wasiojiweza katika jamii yetu. Kadhalika, Bwana anamtaka kila mtu katika jamii yetu kujenga utamaduni wa kuwajibika, kuishi ndani ya uwezo wake, uzalendo na kujaliana. Lisipofanya hivi Kanisa na Taifa kwa ujumla litegemee maafa makubwa kama vile ukame, njaa, mafuriko, vita na umasikini mkubwa zaidi.

Kama vile Mungu alivyolionya kanisa la Efeso Bwana analiambia Kanisa la Tanzania ya kwamba, ” umeuacha upendo wa kwanza. Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; utubu. Usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake” [Ufunuo 2:4]

Tangia mwaka 2009 nimekuwa nikitekeleza jukumu la kutangaza habari njema ya uamsho mkubwa wa kiuchumi utakaoanzia Kanisani na kusambaa katika jamii nzima ya Tanzania na Barani Afrika. Jukumu hilo lilifuatia maono ambayo Bwana alinionyesha tangia mwaka 2004 tulipokuwa kwenye maombi ya muda mrefu huko Uingereza.

Pamoja na habari hizo njema Bwana amekuwa makini kutuonya kwamba uamsho huo mkubwa utatanguliwa na mtikisiko mkubwa wa kiuchumi. Hii ni kwa sababu misingi mibovu ya kiuchumi iliyojengeka kwa muda mrefu ni lazima ibomolewe kwanza. Miaka zaidi ya saba iliyopita Bwana alisema viongozi, biashara na taasisi kadhaa kongwe zilizozoea mfumo potofu wa kiuchumi zitatikiswa kiasi ambacho kila mmoja atajiuliza kulikoni. Nilisema wengi watasikitika na kuhamaki lakini kwa watakao amini ujumbe huu hawatakuwa na sababu ya kuogopa bali watafurahi kwani wanajua hayo hayana budi kutokea kabla uamsho wenyewe haujajiri. Hali ngumu ya kiuchumi tunayoiona hivi sasa hapa kwetu Tanzania, chokochoko za vita zinazoendelea duniani na maafa ya njaa yanayozikumba baadhi ya nchi za Afrika ni mwanzo tu wa utungu wenyewe. Ukweli ni kwamba – kama hatubadilika haraka – tutegemee maumivu makali zaidi huko mbeleni.

Kwa kuwa uamsho huu utaanzia Kanisani mtikisiko mkubwa ni lazima pia uanzie Kanisani. Kama vile Kristo alivyoingia hekaluni na kupindua meza za watu walioigeuza nyumba yake ya sala kuwa pango la wanyang’anyi Bwana ataanza kutakasa Kanisa lake kwa kubomoa mafundisho, itikadi na tamaduni potofu juu ya mafanikio. Wakati sakata hilo likiendelea katika jamii yetu Bwana ataleta mtikisiko mkubwa wa kiuchumi duniani kote hususan Marekani na Ulaya. Maafa ya kimazingira (ukame, mafuriko, njaa n.k) pia vitatokea ikiwa ni pamoja na kusababisha machafuko makubwa ya kisiasa. Kwa kuwa karibu kila nchi itakuwa na majanga yake Bara la Afrika – kwa kuwa tegemezi wa misaada kutoka nje – litaathirika zaidi kwani halitakuwa na uwezo wa kuhimili mtikisiko huo mkubwa.

Kwa kifupi misingi mibovu ya kiuchumi ambayo Bwana anataka ibomolewe ni ibada ya sanamu (kuabudu miungu mingine hususan shetani), kutokuwajibika, kutegemea misaada, ubinafsi na ubadhirifu. Pengine dhambi kubwa zaidi (au niseme dalili ya uhakika zaidi inayoashiria dhambi hizo hapo juu) ni kutokuwajali masikini wasiojiweza. Kanuni ya mafanikio inatutaka kutumia nyenzo tulizopewa na Mungu kufanya kazi kwa bidii ili kutatua matatizo, kukidhi uhitaji na kuboresha maisha ya wengine. Msingi wa Imani ya Kikristo ni kujaliana sisi kwa sisi hususan wasiojiweza. Kristo alisema jinsi pekee itakayotuthibitisha kwamba sisi ni wanafunzi wake (Wakristo) wa kweli ni jinsi tunavyopendana. Yesu Kristo na Mitume wake walikuwa na hazina maalum kwa ajili ya masikini wasiojiweza. Hivi ndivyo Kanisa la mwanzo lilivyofuta umasikini miongoni mwao na kuvutia mafanikio ya kila namna. [Yohana 13:34-35; Matayo 25: 30-40; Matendo 4:32-37; Yakobo 1: 17]

Kanisa ni Ubalozi wa Kristo na linapaswa kuwa kitovu cha mafanikio na kimbilio la wanyonge. Inasikitisha kuona Makanisa ya Afrika – hususan madhehebu ya Kipentekoste – hivi sasa hayana kabisa utamaduni wa kuwajali masikini. Kanisa tumewaachia wafadhili wa kutoka nje jukumu la kujali watu wetu wasiojiweza. Mbaya zaidi, badala ya kusisitiza theologia ya heshima ya kufanya kazi tumeendekeza mafanikio ya kimiujiza, uvivu na utegemezi kiasi cha hata sisi sote tulio na uwezo wa kujiletea maendeleo yetu kudai haki ya kusaidiwa.

Kanisa lina uwezo wa kifedha na ki-miundo-mbinu wa kutokomeza umasikini, ukandamizaji, maradhi na matatizo mengine sugu yanayoikabili jamii yetu tena ndani ya muda mfupi sana. Lakini cha kusikitisha ni kwamba wakati Kanisa na viongozi wake wanaogelea kwenye utajiri wanajamii – wakiwemo wengi wa waumini wao – wanazama katika umasikini, ujinga na maradhi. Kutokana na kukosa maadili na upendo wa Kristo ufa wa kimaisha kati ya taasisi za kidini na wananchi wanaozizunguka unazidi kupanuka siku kwa siku. Ni jambo la kawaida kabisa siku za leo kuona viongozi (wa Makanisa au Huduma) wenye vyeo na majina makubwa wakiishi kwenye majumba ya kifahari wakati washirika wao wanalala nje. Watumishi wengi hatuoni aibu kumiliki vyombo vya usafiri vya kifahari wakati washirika wetu hawana hata nauli ya daladala ya kumpeleka mtoto hospitali. Wakati tunapendeza kwa kuvaa mavazi ya bei mbaya na kunawiri kwa kula nyamachoma hatujali kuona wajane, yatima na walemavu wakitembea uchi ama kulala njaa.

Kristo Yesu hapingi dhana ya Watumishi au huduma wanazoziongoza kuwa matajiri au kuishi maisha ya mafanikio. Yeye mwenyewe hakuishi maisha ya kimasikini na wala hakuwafundisha wanafunzi wake kuishi maisha ya kubangaiza. Anachotamani kukiona Kristo ni sisi watumishi na taasisi zetu kutumia raslimali ambazo Bwana anatupa ili kuboresha maisha ya wanajamii wetu wote. Kitu ambacho naamini si sahihi ni kuendekeza tofauti kubwa ya kimaisha kati ya Kanisa na viongozi wake kwa upande mmoja na wanajamii kwa upande mwingine. Mbaya zaidi ni pale Kanisa linapoonekana kuwatumia waumini wake kama ngazi ya kupandia kuelekea kwenye kilele cha mafanikio yao binafsi. Wanajamii wanapoona viongozi wao wanatumia maandiko ili kuwaghiribu si tu kwamba wanakatishwa tamaa bali wanafikia hatua ya kuwa na mashaka na kweli ya wokuvu wa Kristo. Kwa lugha ya Yohana Mbatizaji Bwana anasema, “hivi sasa shoka limekwisha kuwekwa shinani; kila mti usiozaa matunda mazuri utakatwa na kutupwa motoni.”

Toba ni kubadilika, kuacha kufanya yasiyopashwa na kuanza kufanya yanayopashwa. Kwa hiyo ishara pekee ya toba ya kweli ni kuanza kujali masikini. Nabii Isaya anasema toba (saumu) anayoitaka Bwana sio kulia, kujipiga kifua au kuvaa magunia; Mungu anataka tuwalishe wenye njaa, tuwakaribishe wasio na makazi na tuwavike nguo walio uchi (Isaya 58). Yohana Mbatizaji pia alisema, “mwenye kanzu mbili na ampe asiye na kanzu; na mwenye vyakula na afanye vivyo hivyo” ili kuonyesha kwamba kweli wametubu. [Luka 3: 7-14].

Ili tufufue uchumi wetu na kuepuka ghadhabu ya Mungu Kanisa ni lazima tujenge utamaduni wa kukidhi uhitaji miongoni mwetu kwa kutumia nyenzo tulizonazo. Kila Mkristo ni vema ajenge utamaduni wa kufanya kazi kwa bidii na kuwajali masikini. Hii ni pamoja na kutenga sehemu fulani ya kipato chetu kwa ajili hii. Kila Mkristo ni vema aabudu na kutoa zaka zake mahali ambapo – pamoja na mambo mengine – pana utamaduni wa kusaidia masikini. Kuabudu na kuendelea kutoa sadaka zako mahali ambapo misingi ya Kikristo haiheshimiwi ni kuvutia laana.

Pamoja na kuwa kituo cha ibada ya kweli Kanisa linapaswa kuwa kitovu cha maendeleo ya jamii. Hii ni pamoja na kusisitiza umuhimu wa elimu, sayansi na teknolojia, maadili mema ya kazi, biashara na uongozi. Lakini jambo muhimu zaidi ni kupalilia moyo wa upendo – kujaliana sisi kwa sisi na hususan wasiojiweza. Kanisa ni lazima liwe na mikakati endelevu ya ustawi wa jamii, ikiwa ni pamoja na kuwa na hazina ya mahitaji ya dharura kama vile chakula, mavazi, na madawa.

Ninaamini wengi wetu tunampenda Mungu na tunatamani kumpendeza yeye. Hatujafanya tuliyopashwa kwa kutokujua na tuko tayari kujirudi. Ndiyo maana Bwana mwenye rehema nyingi ametuma ujumbe huu na yuko tayari kutupatia na Roho wake kutusaidia. Ni kwa sababu hii nachagua kuamini kwamba muda si mrefu Kanisa, Taifa na Bara letu litanufaika na mafanikio makubwa ambayo kwa kweli sote tunayatamani sana.

Dream Life Mission kama sehemu ya Kanisa la Kristo tuna mkakati wetu tuliouita KIMBILIO. Pamoja na utoaji wa mafunzo ya maadili bora ya kazi, biashara na uongozi mkakati wa Kimbilio unalenga kujenga hazina kuu ya Kitaifa ya mahitaji ya dharura. Bwana ametuagiza kujenga hazina ya mahitaji ya kujikimu kama vile chakula, mavazi, malazi na madawa. Kama vile Mungu alivyomuagiza Nuhu kujenga safina na kutunisha hifadhi kabla ya gharika Mungu ametutaka kuweka hifadhi ya kujikimu si tu kwa ajili ya wakati wa maafa ya kitaifa bali kwa ajili ya wahitaji wa kila siku.

Unaweza kupata maelezo zaidi ya jinsi ya kushiriki nasi katika jukumu hili  hapa. Kama uko tayari kuwa mdau wetu tafadhali jaza fomu hii hapa sasa.

Vilevile unaweza kutuma ujumbe huu kwa viongozi wa Kanisa lako au kwa Wakristo  wenzako kwa download na kuprint nakala ya barua hii hapa.

Mungu libariki Kanisa lako, Mungu ibariki Tanzania, Mungu libariki Bara letu la Afrika.

Katika Utumishi,

Balozi NOEL D MATURLU

%d bloggers like this: